Swahili New Testament Bible

Titus 2

Titus

Return to Index

Chapter 3

1

 Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema.

2

 Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikizano, wawe daima wapole kwa kila mtu.

3

 Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukawachukia.

4

 Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu, ulipofunuliwa,

5

 alituokoa. alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali alituokoa kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji.

6

 Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu,

7

 ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uzima wa milele tunaoutumainia.

8

 Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu, wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, ambayo ni mambo mazuri na ya manufaa kwa watu.

9

 Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya Sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu.

10

 Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye.

11

 Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea.

12

 Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi.

13

 Jitahidi kumsaidia mwana sheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji.

14

 Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa.

15

 Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu.

Philemon 1

 

 

 

Please Click the Ads.

Clicking the Ads helps us to keep this free Bible website open for everyone.

Thanks!

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: