Swahili New Testament Bible

Luke 8

Luke

Return to Index

Chapter 9

1

Yesu aliwaita wale kumi na wawili, akawapa uwezo juu ya pepo wote, na uwezo wa kuponya wagonjwa.

2

Halafu akawatuma waende kuhubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.

3

Akawaambia, "Mnaposafiri msichukue chochote: msichukue fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala hata koti la ziada.

4

Nyumba yoyote mtakayoingia na kukaribishwa, kaeni humo mpaka mtakapoondoka katika kijiji hicho.

5

Watu wakikataa kuwakaribisha, tokeni katika mji huo, nanyi mnapotoka kung`uteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao."

6

Basi, wakaanza safari, wakapitia vijijini wakihubiri Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali.

7

Sasa, mtawala Herode, alipata habari za mambo yote yaliyokuwa yanatendeka, akawa na wasiwasi kwa vile walikuwa wakisema: "Yohane amefufuka kutoka wafu!"

8

Wengine walisema kwamba Eliya ametokea, na wengine walisema kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amerudi duniani.

9

Lakini Herode akasema, "Huyo Yohane nilimkata kichwa; sasa ni nani huyu ninayesikia habari zake?" Akawa na hamu ya kumwona.

10

Wale mitume waliporudi, walimweleza yote waliyoyafanya. Yesu akawachukua, wakaenda peke yao mjini Bethsaida.

11

Lakini wale watu walipojua alikokwenda, walimfuata. Yesu akawakaribisha akawazungumzia juu ya Ufalme wa Mungu, akawaponya wale waliohitaji kuponywa.

12

Jua lilipokuwa linaanza kutua, wale kumi na wawili walimwendea wakamwambia, "Waage watu waende kwenye vijiji na mashamba ya karibu, wakajipatie chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tulipo ni nyikani."

13

Lakini Yesu akawaambia, "Wapeni ninyi chakula." Wakamjibu, "Hatuna chochote ila mikate mitano na samaki wawili. Labda twende wenyewe tukawanunulie chakula watu wote hawa!"

14

(Walikuwepo pale wanaume wapatao elfu tano.) Basi, Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Waambieni watu waketi katika makundi ya watu hamsinihamsini."

15

Wanafunzi wakafanya walivyoambiwa, wakawaketisha wote.

16

Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu.

17

Wakala wote, wakashiba; wakakusanya makombo ya chakula, wakajaza vikapu kumi na viwili.

18

Siku moja, Yesu alikuwa anasali peke yake, na wanafunzi wake walikuwa karibu. Basi, akawauliza, "Eti watu wanasema mimi ni nani?"

19

Nao wakamjibu, "Wengine wanasema kuwa wewe ni Yohane mbatizaji, wengine wanasema wewe ni Eliya, hali wengine wanasema kuwa wewe ni mmoja wa manabii wa kale ambaye amefufuka."

20

Hapo akawauliza, "Na ninyi je, mwasema mimi ni nani?" Petro akajibu, "Wewe ndiwe Kristo wa Mungu."

21

Halafu Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hiyo.

22

Akaendelea kusema: "Ni lazima Mwana wa Mtu apate mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na walimu wa Sheria; atauawa, lakini siku ya tatu atafufuliwa."

23

Kisha akawaambia watu wote, "Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate.

24

Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; lakini atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayaokoa.

25

Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe?

26

Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu.

27

Nawaambieni kweli, kuna wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu."

28

Yapata siku nane baada ya kusema hayo, Yesu aliwachukua Petro, Yohane na Yakobo, akaenda nao mlimani kusali.

29

Alipokuwa akisali, sura yake ilibadilika, mavazi yake yakawa meupe na kung`aa sana.

30

Na watu wawili wakaonekana wakizungumza naye, nao ni Mose na Eliya,

31

ambao walitokea wakiwa wenye utukufu, wakazungumza naye juu ya kifo chake ambacho angekikamilisha huko Yerusalemu.

32

Petro na wenzake walikuwa wamelemewa na usingizi mzito, hata hivyo waliamka, wakauona utukufu wake, wakawaona na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye.

33

Basi, watu hao wawili walipokuwa wakiondoka, Petro alimwambia Yesu, "Bwana, ni vizuri kwamba tupo hapa: basi, tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya."--Kwa kweli hakujua anasema nini.

34

Petro alipokuwa akisema hayo, mara wingu likatokea na kuwafunika; na wingu hilo lilipowajia, wale wanafunzi waliogopa sana.

35

Sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: "Huyu ndiye Mwanangu niliyemchagua, msikilizeni."

36

Baada ya hiyo sauti kusikika, Yesu alionekana akiwa peke yake. Wanafunzi walikaa kimya juu ya tukio hilo, na wakati ule hawakumwambia mtu yeyote mambo hayo waliyoyaona.

37

Kesho yake walipokuwa wakishuka kutoka kule mlimani, kundi kubwa la watu lilikutana na Yesu.

38

Hapo, mtu mmoja katika lile kundi akapaaza sauti, akasema, "Mwalimu! Ninakusihi umwangalie mwanangu--mwanangu wa pekee!

39

Pepo huwa anamshambulia, na mara humfanya apige kelele; humtia kifafa, na povu likamtoka kinywani. Huendelea kumtesa sana, asimwache upesi.

40

Niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze, lakini hawakuweza."

41

Yesu akasema, "Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini?" Kisha akamwambia huyo mtu, "Mlete mtoto wako hapa."

42

Wakati mtoto huyo alipokuwa anamjia Yesu, yule pepo alimwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu akamponya mtoto na kumkabidhi kwa baba yake.

43

Watu wote wakashangazwa na uwezo mkuu wa Mungu. Wale watu walipokuwa bado wanashangaa juu ya mambo yote aliyofanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake,

44

"Tegeni masikio, myasikie mambo haya: Mwana wa Mtu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu."

45

Lakini wao hawakuelewa maana ya usemi huo. Jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao ili wasitambue; nao wakaogopa kumwuliza juu ya msemo huo.

46

Kukatokea majadiliano kati ya wale wanafunzi kuhusu nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi.

47

Yesu aliyajua mawazo yaliyokuwa mioyoni mwao; basi akamchukua mtoto mdogo akamweka karibu naye,

48

akawaambia, "Mtu yeyote anayempokea mtoto huyu mdogo kwa jina langu, ananipokea mimi; na yeyote anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Maana yule aliye mdogo kuliko wote kati yenu ndiye aliye mkubwa kuliko wote."

49

Yohane alidakia na kusema, "Bwana, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu."

50

Lakini Yesu akamwambia, "Msimkataze; kwani asiyepingana nanyi yuko upande wenu."

51

Wakati ulipokaribia ambapo Yesu angechukuliwa juu mbinguni, yeye alikata shauri kwenda Yerusalemu.

52

Basi, akawatuma wajumbe wamtangulie, nao wakaenda wakaingia kijiji kimoja cha Wasamaria ili wamtayarishie mahali.

53

Lakini wenyeji wa hapo hawakutaka kumpokea kwa sababu alikuwa anaelekea Yerusalemu.

54

Basi, wanafunzi wake, kina Yohane na Yakobo, walipoona hayo, wakasema, "Bwana, wataka tuamuru moto ushuke kutoka mbinguni uwateketeze?"

55

Lakini yeye akawageukia, akawakemea.*fa*

56

Wakatoka, wakaenda kijiji kingine. gani mliyo nayo; kwa maana Mwana wa Mtu hakuja kuyaangamiza maisha ya watu, bali kuyaokoa."

57

Walipokuwa wakisafiri njiani, mtu mmoja akamwambia Yesu, "Nitakufuata kokote utakakokwenda."

58

Yesu akasema, "Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia."

59

Kisha akamwambia mtu mwingine, "Nifuate." Lakini huyo akasema, "Bwana, niruhusu kwanza niende kumzika baba yangu."

60

Yesu akamwambia, "Waache wafu wazike wafu wao; bali wewe nenda ukatangaze Ufalme wa Mungu."

61

Na mtu mwingine akamwambia, "Nitakufuata, lakini niruhusu kwanza nikawaage wale walio nyumbani kwangu."

62

Yesu akamwambia, "Yeyote anayeshika jembe tayari kulima na huku anaangalia nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu."

Luke 10

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Software is Available At These Sites: